News

Posted On: Mar, 28 2025

Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Lakutana Morogoro

News Images

Wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wanakutana mkoani Morogoro kujadili na kupitisha bajeti ya Bodi ya Mfuko wa Barabara kwa mwaka wa fedha wa 2025/26.

Akiongea na Waandishi wa Habari mkoani humo, Mwenyekiti wa Baraza hilo na Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga, amesema kuwa bajeti hiyo imezingatia majukumu makubwa ya Bodi kwa kutoa kipaumbele kwenye uanishaji wa vyanzo vipya vya mapato ya Mfuko wa Barabara, ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za matengenezo ya Barabara zinazopelekwa kwa Wakala za Barabara nchini (TANROADS na TARURA) pamoja nakuhakikisha fedha zinazokusanywa kwa ajili ya matengenezo ya barabara zinapelekwa kwa wakati kwa Wakala za Barabara ili mtandao wa barabara nchini wenye jumla ya kilomita 188000 uweze kupitika katika majira yote ya mwaka.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Idara ya Mipango na Mapato wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Godlove Stephen, amesema kuwa bajeti ya mwaka wa fedha 2025/26 imejikita katika kufanya tafiti mbali mbali zitakazowezesha upatikanaji wa vyanzo vipya vya mapato ya Mfuko wa Barabara ili kuongeza uwezo wa Mfuko katika kugharamia mategenezo ya Barabara hapa nchini, kuimarisha usimamizi wa makusanyo yatokanayo na hifadhi za barabara pamoja na kuboresha matumizi yake kwa lengo la kuongeza fursa za ajira na kipato kwa Watanzania watakaopenda kutumia hifadhi za barabara katika kufanya biashara mbali mbali ili kujikwamua kiuchumi.

Nae Rehema Lungo, akizungumza kwa niaba ya wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara amesema kuwa bajeti hiyo ya Bodi ya Mfuko wa Barabara imepita bila kupingwa na kwamba wao kama watumishi wa Bodi wanajipanga kwa ajili ya kuandaa Mpango Kazi sambamba na kuainisha manunuzi yote kwenye mfumo wa manunuzi wa NeST kwa ajili ya kuanza utekelezaji wa bajeti hiyo ifikapo Julai 1, 2025.