Historia na Majukumu ya Bodi
Historia ya Bodi
Sheria ya Tozo za Barabara ya 1985 iliyoanzishwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania mnamo tarehe 26/07/1985 iliidhinisha makusanyo ya tozo katika magari yanayotumia Barabara za umma na tozo zote zinahusiana na makusanyo katika Barabara. Makusanyo hayo yalichukuliwa kama makusanyo ya kawaida ya Serikali. Mifuko miwili ya Barabara ilianzishwa kwa azimio tofauti lililofanywa na Waziri wa Fedha kwa nyakati tofauti. Azimio la kwanza liliitwa “AZIMIO LA KUANZISHA MFUKO MAALUMU WA FEDHA ZA BARABARA” Au “MFUKO WA BARABARA” lilifanyika mnano mwezi wa Nane 1991, na la pili AZIMIO LA KUANZISHA MFUKO WA BARABARA WA SERIKALI ZA MITAA” lilifanyika mwezi wa Nane 1992. Mfuko wa Barabara ulilenga matengenezo ya Barabara kuu pamoja na matengenezo ya Barabara za Mijini na vijijini. Makusanyo yalilenga kutokana na tozo katika mafuta ya Dizeli ,Petroli pamoja na tozo kutoka katika vyanzo vingine kama vile Leseni za Magari na usajili wa Magari.
Kulingana na kuanzishwa tozo katika mafuta ya dezeli na petroli katika Ibara ya 17 ” Sheria ya Hazina na Ukaguzi” (sura ya 439) ambayo inaipa mamlaka Serikali kuanzisha mfuko maalum , na kutokana na taratibu za utawala Azimio halikuwa na nguvu ya kisheria hivyo hakukuwa na uwajibikaji katika Azimio, hivyo ili kuupa mfuko nguvu ya kisheria na kupata nguvu katika kufadhili matengenezo ya Barabara na usimamizi wa mfuko , Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilifanya marekebisho ya sheria za Barabara (Namba 2) ya mwaka 1998 ambayo ilianzisha Mfuko wa Barabara na Bodi ya Mfuko wa Barabara. Sheria hii ilifanyiwa marekebishokwa nyakati tofauti na kwa sasa inatumika kama sheria ya Tozo za Barabara na Mafuta Sura 220 (iliyofanyiwa marekebisho 2019).
Bodi ilianza kufanya kazi mwaka 2000 katika jengo la TETEX Barabara ya Pamba Dar es salaam.
Mwenyekiti wa kwanza wa Bodi ya Mfuko wa Barabara alikuwa Rose Mang’enya, aliyefuatiwa na Philipo A.Magani na Joseph O. Haule. Kwa sasa Bodi inaendeshwa na Makamu Mwenyekiti Octavian Mshiu
Majukumu ya Bodi
Kutokana na kifungu cha 5(4) cha Sheria ya Tozo za Barabara na Mafuta, Sura ya 220, Bodi ya mfuko wa Barabara ina majukumu makuu yafuatayo:
- Kumshauri Waziri mwenye dhamana ya Barabara juu ya vyanzo vipya vya mapato ya Mfuko, marekebisho ya viwango ya vyanzo vilivyopo na kanuni za ukusanyaji wa mapato ya Mfuko kwa dhumuni la kuhakikisha uwepo wa mapato ya kutosha na endelevu kwa ajili ya shughuli za barabara;
- Kutumia fedha za Mfuko kwa makusudi yaliyoidhinishwa na Bunge;
- Kuweka na kutoa utaratibu utakaotumiwa na wakala wa ukusanyaji mapato ya Mfuko;
- Kuhakikisha kuwa mapato yote ya Mfuko yamekusanywa na kupelekwa kwenye akaunti ya Mfuko;
- Kutengeneza au kurekebisha, utaratibu wa ugawaji wa fedha za Mfuko na kumshauri Waziri mwenye dhamana ya Barabara kuhusu utaratibu huo;
- Kumshauri Waziri mwenye dhamana ya barabara juu ya ugawaji wenye ufanisi wa fedha za Mfuko;
- Kugawa fedha za Mfuko kwa Wakala wa Barabara;
- Kuhakikisha kuwa shughuli za kiufundi na kifedha za Wakala wa Barabara na Mfuko wenyewe zinafanyika kwa ufanisi mkubwa;
- Kufuatilia matumizi ya fedha zilizopelekwa kwa Wakala wa Barabara ili kuhakikisha kuwa zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na Mfuko;
- Kuteua Mtendaji Mkuu wa Mfuko na Maafisa Wandamizi;
- Baada ya uhakiki wa mkaguzi mkuu wa Hesabu za serikali kuteua, mkaguzi atakayekagua hesabu za Mfuko; na
- Kutoa mapendekezo mengine yoyote kwa Waziri wa Barabara yatakayoonekana ni muhimu ili kuiwezesha Bodi kutimiza malengo yake.