News

Posted On: Apr, 15 2024

Bodi ya Mfuko wa Barabara Yaonya TANROADS na TARURA Fedha za Matengenezo

News Images

Bodi ya Mfuko wa Barabara, imezitaka Wakala ya Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) kuhakikisha wanatumia fedha za matengenezo ya barabarazinazotolewa na Mfuko wa Barabara kama ilivyoelekezwa.

Akizungumza mkoani Morogoro Aprili 15, 2024 mara baada ya kufanyika kwa Uchaguzi wa Katibu na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Bodi hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara, Mhandisi Rashid Kalimbaga amesema kuwaBodi itahakikisha inazigawa fedha hizo kwa wakati kwa wakala wa barabara ilikusaidia matengenezo ya barabara kufanyika kwa haraka.

"Sisi kama Bodi jukumu letu kuu ni kuahakilisha mara tu tunapopata fedha, tunazigawa kwa TANROADS na TARURA na haifiki siku tatu fedha hizo zinakuwa zimefika kwao", amesema Kalimbaga.

Aidha, Kalimbaga ameongeza kuwa hadi kufikia Mwezi Machi, 2024 kiasi cha shilingi Bilioni 110 kimetolewa kwa TANROADS na shilingi Bilioni 89 kwa TARURA kwa ajili ya matengenezo ya barabara nchi nzima na kusisitiza Bodi inaendelea kutoa fedha kwa kadri inayoletewa kutoka Hazina.

Kalimbaga amefafanua kuwa Bodi inaendelea kufuatilia kwa makini kuhakikisha fedha wanazozitoa zinakwenda kuhudumia yale yaliyokusudiwa na Bodi hiyo.

Kuhusu uanzishwaji wa Baraza hilo, Kalimbaga amesema kuwa watatumia Baraza hilo kuhakikisha wanajadili na kuzifanyia kazi hoja za watumishi pamoja na kuhakikisha motisha na stahiki kwa watumishi zinapatikana ili kuleta ari na kasi ya utendaji kazi wa Bodi.

Baraza la Wafanyakazi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara linatarajiwa kuzinduliwa wiki ijayo na Waziri wa Ujenzi,Innocent Bashungwa ambapo hatua za awali za uzinduzi huo zimefanyika mkoani Morogoro leo Aprili 15, 2024 kwa Bodi hiyo kufanya uchaguzi wa Katibu na Wajumbe wa Baraza hilo.