News

Posted On: Apr, 06 2024

​Miaka 3 ya Dkt. Samia na Hali ya Mtandao wa Barabara Nchini

News Images

Mtandao wa barabara hapa nchini una jumla ya kilometa 181,602.2 zikijumisha kilometa 37,225.7 za barabara za Kitaifa na kilometa 144,376.5 za barabara za Wilaya.Barabara za Kitaifa zinasimamiwa na TANROADS na barabara za Wilaya zinasimamiwa na TARURA.

Kutokana na hali ya jiografia ya nchi yetu, usafiri wa barabara ndiyo njia inayotumiwa zaidi kwa usafiri na usafirishaji.Inakadiriwa kuwa zaidi ya asilimia 90 na 80 ya abiria na mizigo, mtawalia, hutumia barabara.

Hivyo ufanisi wa mipango ya Serikali inayolenga maendeleo ya vijijini, uzalishaji wa ajira, maendeleo ya viwanda, kwa kiasi kikubwa, unachangiwa na ubora wa huduma za usafiri wa barabara.

Aidha, miundombinu ya barabara ndiyo rasilimali ya umma yenye thamani kubwa zaidi.Thamani yake inakadiriwa kufikia Shilingi Trilioni 39.5 – sawa na asilimia 23 ya Pato la Taifa.

Juhudi za Serikali katika kuboresha hali miundombinu yabarabara nchini

Kwa kutambua thamani na umuhimu wa barabara kwa maendeleo ya kijamii na kiuchumi, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan, imekuwa ikiimarisha uwezo wa kifedha na kitaasisi ili kuzilinda barabara kwa lengo la kuziwezesha kutumika kwa muda uliopangwa.

Katika kipindi cha miaka mitatu ya uongozi wake, Rais Dkt Samia Suluhu Hassan amekuwa akitenga wastani wa Shilingi bilioni 850 kila mwaka kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara hapa nchini.Fedha hizi zimewezesha utekelezaji wa wastani wa miradi 620 ya matengenezo ya barabara kwa barabara za Kitaifa na miradi 850 kwa barabara za Wilaya kila mwaka.

Aidha, Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikiimarisha uwezo wa taasisi zinazosimamia kazi za barabara, hususan TANROADS, TARURA na Bodi ya Mfuko wa Barabara, kwa kuziongezea vitendea kazi pamoja na wataalam.

Kuimarika kwa uwezo wa kifedha na kitaasisi kumewezesha matengenezo ya barabara kufanyika mara kwa mara.Kutokana na kufanyika kwa matengenezo hayo, zaidi ya asilimia 90 ya mtandao wa barabara za Kitaifa uko kwenye hali nzuri na wastani.Aidha zaidi ya asilimia 60 ya mtandao wa barabara za Wilaya uko kwenye hali nzuri na wastani.Hivyo sehemu kubwa ya mtandao wa barabara unapitika kipindi chote cha mwaka.Hali hii imeiwezesha Tanzania kuwa moja ya nchi za Afrika zenye mtandao bora wa barabara ambao sehemu kubwa inapitika majira yote.

Hata pale mawasiliano ya barabara yanapokuwa yamekatika kutokana na mafuriko, Serikali ya Awamu ya Sita imekuwa ikitoa fedha mara moja ili kurudisha mawasiliano kwa wakati na hivyo kuwawezesha wananchi kuendelea na shughuli zao za kijamii na kiuchumi.Mfano ni kazi za dharura zilizofanyika maeneo ya Hanang (Manyara), Liwale (Lindi) na Ununio (Dar es Salaam).

Kwa kuboresha miundombinu ya barabara, wananchi wamewezeshwa kuzifikia huduma za kijamii na kiuchumi zinazotolewa na Serikali ya Awamu ya Sita kama vile elimu, afya, masoko, ajira na fursa nyingine za kujipatia kipato.

Heko kwa Serikali ya Awamu ya Sita, chini ya uongozi mahiri wa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuweka mkazo katika kuimarisha miundombinu ya barabara na hivyo kuiwezesha kutoa mchango unaotarajiwa kwenye maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

­­­­­­­­­­­­Usimamizi na ugharamiaji wa matengenezo ya barabara

Barabara zikishajengwa uhitaji kufanyiwa matengenezo kikamilifu ili kulinda thamani yake, uwekezaji wa Serikali na kuziwezesha kutumika kwa muda uliopangwa.Hii ni kwa sababau ubora wa barabara hupungua kutokana na kuzeeka, uzito wa magari na athari za mabadiliko ya tabianchi.Matengenezo yasipofanyika kikamilifu, barabara uharibika mapema na hivyo kupoteza thamani yake, thamani ya uwekezaji wa Serikali na kuongeza gharama za usafiri na usafirishaji.

Matengenezo ya barabara hapa nchini yanasimamiwa na kugharamiwa chini ya Sheria ya Tozo za Barabara na Mafuta, Sura 220.Chini ya Sheria hii, Serikali iliunda Mfuko wa Barabara na Bodi yake mwaka 2000 ili kuhakikisha uwepo wa kutosha na endelevu wa fedha za kugharamia matengenezo ya barabara. Serikali ilianzisha Mfuko wa Barabara kama moja ya mifuko maalum chini ya Ibara ya 135(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Serikali ilianzisha Mfuko na Bodi yake kama njia ya kutatua changamoto kubwa ya ubovu wa mtandao wabarabara kati ya miaka ya 1980 na 1990 kutokana na kutofanyiwa matengenezo kikamilifu.Nchi nyingi za Afrika zilianzisha mifuko ya aina hii na hadi sasa kuna nchi 34 zenye mifuko hiyo.

Kwa mujibu wa Sheria, majukumu makuu ya Bodi ni kuhakikisha upatikanaji wa fedha za kutosha za kugharamia matengenezo, kugawa fedha hizo kwa Wakala za Barabara na kufuatilia matumizi ya fedha hizo.

Tozo ya mafuta ni chanzo kikuu cha mapato ya Mfuko kwani huchangia wastani wa asilimia 96 ya mapato yote ya Mfuko. Tozo ya mafuta kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara ni TZS 263 kwa kila lita ya petroli na dizeli.Vyanzo vingine ni ushuru wa magari ya kigeni (transit charges) na Tozo ya uzidishaji wa uzito.

Kwa mujibu wa Kifungu cha 4(2) cha Sheria ya Barabara na Mafuta, Sura ya 220,makusanyo yote ya Mfuko wa Barabara yanatakiwa yawekwe kwenye akaunti ya Mfuko wa Barabara inayosimamiwa na Bodi.Hii ni kwa sababu mapato hayo yametengwa mahususi (ring-fenced) kwa ajili ya kugharamia matengenezo ya barabara za Kitaifa na Wilaya zinazosimamiwa na TANROADS na TARURA, mtawalia.

Moja ya mafanikio makubwa ya kuanzishwa kwa Mfuko wa Barabara na Bodi yake ni kuimarika kwa ubora wa mtandao wa barabara hapa mchini.Barabara za Kitaifa zilizo kwenye hali nzuri zimeongezeka na kufikia wastani wa asilimia 90 kutoka wastani wa asilimia 13 mwaka 2000.Aidha, barabara za Wilaya zilizo kwenye hali nzuri na wastani zimeongezeka na kufika asilimia 60 toka asilimia 10 mwaka 2000.

Bodi ya Mfuko wa Barabara itaendelea kufanya kazi kwa juhudi na umahiri ili kutoa mchango unaotarajiwa ili kufikia malengo ya Serikali ya Awamu ya Sita.