News
Watumishi Tunzeni Siri za Serikali

Watumishi wa Bodi ya Mfuko wa Barabara wametakiwa kuzingatia miiko na utunzaji siri za Serikali pamoja na kuongeza ari ya utendaji kazi katika utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku.
Akizungumza katika kikao cha Wajumbe wa Menejimenti na Watumishi wa Bodi ambacho kimefanyika kwa siku mbili mkoani Singida, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Ludovick nduhiye, amewaagiza watumishi wa Bodi kutunza siri za Serikali kwani utoaji siri za Serikali ni jambo la hatari ambalo linaweza kusababisha taharuki kwa jamii.
“Mambo ya ndani ya Serikali mtu akianza kuyatoa nje ni shida, kila kitu kinaenda kwa kusudi maalumu kwa hiyo tusiseme yale ambayo hatujatumwa kusema, tuwe watumishi mahiri tuzingatie maadili ya Utumishi wa Umma”, amesema Nduhiye.
Ameongeza kuwa, kikao hicho kitawasaidia watumishi kubadilishana uzoefu, kujenga mshikamano baina yao na hivyo kuchochea morali na ari ya kazi kwa watumishi jambo litakalongeza tija na ufanisi katika utendaji kazi wa Bodi.
Kwa upande wake Kaimu Meneja Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga, amesema kuwa katika kikao hicho yametolewa pia mafunzo yanayolenga kuwakumbusha watumishi wajibu wa kila siku wanapokuwa kazini ili kuwaongezea tija na ufanisi katika utendaji kazi wao wa kila siku.
Nao baadhi ya Viongozi na Watumishi walioshiriki kikao hicho wameelezea umuhimu wa mafunzo hayo ikiwemo umuhimu wa utunzaji siri na madhara ya kutofanya hivyo, huku wakiupongeza uongozi wa Bodi kwa kuona haja ya kuwa na kikao hicho cha faragha ambacho wanaamini kitakuwa mwarobaini wa kuondoa dosari zinazoweza kujitokeza katika utendaji kazi wa kila siku.
Kikao hicho kimefunguliwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Sekta ya Ujenzi) Ludovick nduhiye.