Habari

Imewekwa: Feb, 15 2026

Bilioni 12.8 Zatumika Matengenezo ya km 13.1 za Barabara ya Iringa–Mtera

News Images

Barabara ya Iringa–Mtera, ambayo ni kiungo muhimu kinachounganisha jamii, biashara na huduma za kijamii, imefanyiwa matengenezo makubwa yenye lengo la kuboresha usalama, ufanisi na uimara wake.

Kwa mujibu wa Taarifa Fupi ya Matengenezo ya Barabara ya Iringa–Mtera, iliyosomwa na Meneja wa TANROADS Mkoa wa Iringa, Mhandisi Yudas Msangi, mradi huo umehusisha matengenezo ya jumla ya kilometa 13.1 kwa gharama ya Shilingi bilioni 12.8.

Taarifa hiyo imewasilishwa mbele ya wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabarawakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhandisi Mussa Natty, pamoja na Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara na Rais wa Chama cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika (ARMFA), Mhandisi Rashid Kalimbaga, wakati wa ziara yao ya kukagua utekelezaji wa kazi za matengenezo ya barabara.

Akitoa maelezo ya kina, Mhandisi Msangi amesema kazi zilizotekelezwa ni pamoja na kuziba mashimo, kuimarisha tabaka la juu la barabara, kuboresha mifumo ya mifereji ya maji na kuweka alama za barabarani kwa lengo la kuongeza usalama kwa watumiaji wa barabara.

Ameongeza kuwa maboresho hayo yamechangia kupunguza gharama za uendeshaji wa magari, kupunguza muda wa safari na kurahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo kati ya Iringa na Mtera.

“Zaidi ya kuboresha miundombinu, matengenezo haya yanaakisi dhamira ya kuendeleza usimamizi endelevu wa barabara. Mtandao imara wa barabara ni msingi wa ukuaji wa uchumi, unaowaunganisha wakulima na masoko, kusaidia shughuli za utalii na kuwezesha upatikanaji wa huduma za elimu na afya,” amesema Msangi.

Aidha, Msangi amesema kuwa barabara hiyo ni muhimu kwa Mkoa wa Iringa na Taifa kwa ujumla, kwani inatumika kusafirisha bidhaa kutoka mikoa ya kusini kuelekea kaskazini na kwamba ni sehemu ya mtandao mkubwa wa barabara unaounganisha nchi za kusini na kaskazini mwa Afrika hadi Cairo, Misri.

Utekelezaji wa matengenezo ya Barabara ya Iringa–Mtera unaonesha dhamira ya Serikali kupitia Mfuko wa Barabara kuendelea kuwekeza katika maendeleo ya miundombinu. Kutokana na hali bora ya barabara iliyoboreshwa, wananchi wanaoishi kandokando ya barabara hiyo wanatarajia kunufaika na safari salama zaidi pamoja na fursa pana za kiuchumi.