News

Posted On: Oct, 05 2023

​Bodi ya Mfuko wa Barabara Yafurahishwa na Matengenezo ya Barabara Kigoma

News Images

Bodi ya Mfuko wa Barabara(RFB) imefurahishwa na ubunifu unaofanywa na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Kigoma kwa kutumia kiasi kidogo cha fedha wanazozipata kwa ajili ya matengenezo ya barabara mkoani humo.

Akizungumza kwa niaba ya Bodi Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Barabara Octavian Mshiu, amewaambia waandishi habari mkoani Kigoma kuwa Bodi hiyo imefurahishwa na kazi inayofanywa na TANROADS mkoani humo, ya kupendezesha mji wa Kigoma kupitia uboreshaji wa miundombinu ya barabara na madaraja mkoani humo.

“Tumefurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na TANROADS katika Mkoa huu kwa jinsi ambavyo wamekuwa wabunifu kwa namna wanavyotumia Fedha za Mfuko wa Barabara, kuboresha miundombinu ya barabara katika mji huu wa Kigoma,"ameeleza Mshiu na kuongeza kuwa

“Tumeona njia za chini ya barabara za waenda kwa miguu ili kupunguza ajali zitokanazo na watu kuvuka barabara, hasa wanafunzi, tofauti na barabara za juu za waenda kwa miguu zilizoko Mkoa wa Dar es Salaam, barabara hizi za chini zinatumika na zinapendwa zaidi na watumia barabara wa Mkoa wa Kigoma," amesema Mshiu.

Mshiu ameongeza kuwa RFB imefurahishwa pia na ujenzi wa barabara za njia nne Kigoma Mjini, ili kupunguza foleni kwa magari yanayoingia mjini na kupendezesha mji kwa kujenga maegesho ya magari barabarani ambayo pia yatatumika kama chanzo cha mapato ya fedha za matengenezo ya barabara.

Wakala wa barabara mkoani Kigoma imetumia fedha za matergenezo kufanya matengenezo ya barabara ya njia nne ili kupunguza foleni mjini, kuweka taa za barabarani pia kuweka parking blocks kwa kupendezesha mji, mbao za matangazo za kidigitali (billboard), frame za maduka ndani ya subway na speed camera ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuwa chanzo cha mapato.

Awali akiwasilisha taarifa yake mbele ya Bodi ya Mfuko wa Barabara Meneja wa TANROADS Mkoa wa Kigoma Mhandisi Narcis Choma amesema kuwa Wakala wa barabara mkoani Kigoma imetumia fedha kufanya matengenezo ya barabara ya njia nne ili kupunguza foleni mjini, kuweka taa za barabarani pia kuveka parking blocks kwa kupendezesha mji,

“Tumeweka pia mbao za matangazo za kidigitali (billboards) na vyumba vya maduka ya biashara kwenye njia za waenda kwa miguu zilizo chini ya barabara ili kukusanya fedha za matengenezo ya barabara pamoja na kamera za kudhibiti mwendo ambazo zikitumiwa vizuri zinaweza kuwa chanzo cha mapato”, amesema Choma.

Nae Zaituni Govela mfanyabiashara wa vitumbua katika eneo la Zulu - Gungu kunakojengwa barabara ya chini ya waenda kwa miguu (subway), ameipongeza Serikali kwa ujenzi huo na kuongeza kuwa sasa watakuwa na amani zaidi wanapovuka barabara katika eneo hilo.

Upendezeshaji wa miundombinu ya barabara kwenye miji ni agizo la Katibu Mkuu Ujenzi Balozi Mhandisi Aisha Amour kwa Taasisi za Sekta ya Ujenzi na hasa Wakala wa Barabara.