Habari
Dkt. Msonde: Lindeni Miundombinu ya Barabara ili kulinda Thamani Fedha za Umma
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, amewataka wananchi kuwa mstari wa mbele katika kulinda miundombinu ya barabara kwa kuacha vitendo vya uharibifu vinavyosababisha hasara kwa Serikali na kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Dkt. Msonde ametoa wito huo alipotembelea banda la Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) katika Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nanenane yanayoendelea katika Viwanja vya John Malecela jijini Dodoma, ambapo alipata fursa ya kujionea elimu inayotolewa kuhusu ufadhili wa matengenezo ya barabara na umuhimu wa kuhifadhi miundombinu hiyo.
Amesema Serikali inaendelea kutenga fedha kupitia bajeti ya kila mwaka kwa ajili ya matengenezo ya barabara ili kuhakikisha mtandao wa barabara unabaki katika hali nzuri, unaendelea kutoa huduma bora kwa wananchi na kuchochea ukuaji wa shughuli za kijamii na kiuchumi.
"Barabara hazijengwi tu, bali zinahitaji kutunzwa wakati wote. Matengenezo ya mara kwa mara ndiyo yanayosaidia kuongeza maisha ya barabara na kuhakikisha wananchi wanaendelea kuzitumia kwa usalama," amesema Dkt. Msonde.
Aidha, amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika miundombinu ya usalama barabarani ikiwemo alama za barabarani, taa za kuongozea watumiaji wa barabara na miundombinu mingine muhimu, lakini baadhi ya wananchi wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uharibifu kama kung'oa taa na kuharibu alama za barabarani.
Kwa mujibu wa Dkt. Msonde, vitendo hivyo huongeza gharama za matengenezo kwa Serikali, kwani fedha zinazopaswa kuelekezwa katika kuboresha au kupanua mtandao wa barabara hulazimika kutumika kurekebisha uharibifu unaoweza kuzuilika. Amesema hali hiyo pia huongeza hatari ya ajali na kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara.
Vilevile, amewataka wananchi kuheshimu hifadhi ya barabara kwa kuepuka kuvamia maeneo yaliyotengwa kwa ajili ya upanuzi wa barabara siku zijazo pamoja na kufanya shughuli za biashara ndani ya hifadhi hiyo. Amesisitiza kuwa matumizi yasiyo sahihi ya maeneo hayo huathiri usalama wa barabara, huongeza gharama za matengenezo na huchelewesha utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Dkt. Msonde amesema mafanikio ya Serikali katika kuhakikisha barabara zinabaki salama na zinapitika wakati wote yanategemea ushirikiano wa wananchi katika kuzilinda na kuzitunza.
"Barabara ni mali ya Watanzania wote. Kila mmoja ana wajibu wa kuzilinda ili fedha zinazotengwa kwa ajili ya matengenezo zilete tija kwa wananchi na kuhakikisha miundombinu hiyo inaendelea kuhudumia kizazi cha sasa na kijacho," amesisitiza Dkt. Msonde.