Habari
Rfb yatoa tahadhari kwa watumiaji wa barabara wakati wa mvua za el niño
Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) imewataka watumiaji wa barabara kuchukua tahadhari wakati wa msimu wa mvua za El Niño unaotarajiwa kuanza katika kipindi cha mwisho wa Septemba na kuendelea katika miezi ya Oktoba hadi Desemba 2026.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), mvua hizo zinatarajiwa kuanza katika wiki ya nne ya Septemba hadi wiki ya kwanza ya Oktoba 2026 katika maeneo ya ukanda wa Ziwa Victoria, kabla ya kuenea katika maeneo mengine nchini wakati wa mwezi Oktoba. Maeneo yanayotarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani ni pamoja na ukanda wa Ziwa Victoria, Pwani ya Kaskazini, Nyanda za Juu Kaskazini-Mashariki na maeneo ya Kaskazini mwa Kigoma.
Kutokana na uwezekano wa mvua kubwa na kuongezeka kwa maji, RFB inawakumbusha watumiaji wa barabara kuwa makini hasa wanapokutana na maeneo hatarishi, ikiwemo madaraja, vivuko, makalavati, kingo za barabara, mabonde, maeneo yenye miteremko na milima, pamoja na maeneo yenye utelezi.
RFB inasisitiza tahadhari zifuatazo:
- Madaraja: Usivuke daraja lililojaa maji au lenye maji yanayopita kwa kasi.
- Vivuko: Usivuke maji yenye kasi au yenye kina kisichojulikana.
- Makalavati: Punguza mwendo na jihadhari na maji yanayopita juu ya barabara.
- Kingo za barabara: Epuka kusogea karibu na kingo za barabara, hasa maeneo yenye mmomonyoko.
- Mabonde: Usipite katika maeneo yenye maji mengi au mafuriko.
- Miteremko/Milima: Punguza mwendo na jihadhari na maporomoko ya udongo au mawe.
- Maeneo yenye utelezi: Punguza mwendo na epuka maeneo yenye udongo wa mfinyanzi au maji yaliyotuama.
Bodi inawahimiza wananchi kuzingatia usalama, kupunguza mwendo, kufuata alama na maelekezo ya barabarani, na kuepuka kulazimisha kupita katika maeneo yaliyojaa maji.
Usalama kwanza. Punguza mwendo, chukua tahadhari, fika salama.