News

Posted On: Sep, 27 2023

Waziri Bashungwa Atoa Rai Matumizi ya "BARABARA APP"

News Images

Waziri wa Ujenzi, Innocent Bashungwa, amewataka wananchi kutoa taarifa za hali ya barabara nchini kupitia mfumo wa kielektroniki wa ufuatiliaji wa hali ya barabara maarufu kama ‘Barabara App’ ili hatua za haraka kwa barabara zinazohitaji matengenezo ziweze kuchukuliwa.

Amesema kupitia mfumo huo, watumiaji wa barabara wanaweza kushiriki katika kusimamia miundombinu ya barabara katika maeneo wanayoishi au kupita kwa kutuma taarifa muhimu za hali ya barabara ambazo zitapokelewa moja kwa moja na Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS), Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) na Bodi ya Mfuko wa Barabara itaweza kuziona taarifa hizo na kufuatilia utekelezaji wake.

Amezitaja taarifa hizo ikuwa ni pamoja na barabara kujifunga, daraja au kalvati kubomoka/ kuzolewa na mafuriko, uwepo wa mashimo hatarishi barabarani, kazi za ujenzi wa barabara kufanyika chini ya kiwango, mitaro kuziba pamoja na hujuma zozote zinazofanywa kwenye miundombinu ya barabara.ikiwemo ung'oaji au uibaji wa samani za barabara,

Waziri Bashungwa ameyasema hayo Septemba 27, 2023 jijini Dodoma wakati akihitimisha ziara yake katika Bodi ya Mfuko wa Barabara (RFB) ambapo Waziri huyo alipokea taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi.

“Niwaombe watanzania kutumia mfumo huu unaomwezesha mwananchi kutoa taarifa ya hali ya miundombinu ya barabara yenye changamoto, au hujuma yoyote maeneo anayoishi”, amefafanua Bashungwa.

Bashungwa ameongeza kuwa lengo la kuwa na mfumo huo ni kuipunguzia Serikali gharama kubwa za matengenezo ya barabara ambazo ingeingia kutokana na uchelewaji wa matengenezo hayo.

Aidha, Bashungwa amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita imejipanga vyema kuhakikisha Wakala ya Barabara Nchini (TANROADS) inayosimamia barabara kuu na za mikoa na ile ya Wakala ya Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA), inayosimamia barabara za Halmashauri/ Wilaya wanajipambanua zaidi katika kuhudumia barabara zote nchini.

Amewataka watanzania kuwa na imani na taasisi hizo katika kuhudumia na kusimamia mtandao wa barabara nchini kwa mujibu wa mgawanyo wa majukumu yao.

“Ningependa kuwajulisha watanzania kuwa huko nyuma kulikuwa na maombi makubwa ya barabara ambazo zipo kwenye wilaya zetu ili zipandishwe hadhi kuja TANROADS, lakini hivi sasa hilo hitaji ni kama limeisha kwa sababu TARURA imekwisha jengewa uwezo na kuimarishwa mfuko wake”, amefafanua Bashungwa.

Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Bodi hiyo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara Mhandisi. Rashid Kalimbaga, ameeleza kuwa mbali na mfumo wa kieletroniki wa kufuatilia barabara Bodi imeimarisha mifumo ya usimamizi wa fedha kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuzuia matumizi mabaya ya fedha.

Ameongeza kuwa kuimarika kwa mifumo hiyo kutaziba mianya ya uvujaji wa mapato pamoja na uchakachuaji katika ujenzi na matengenezo ya barabara.