Habari
TANROADS Dodoma Yapokea Bilioni 15.6 Kutoka Mfuko Wa Barabara
Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mkoa wa Dodoma umepokea jumla ya Shilingi Bilioni 15.6 hadi kufikia mwezi Februari 2026 kutoka Mfuko wa Barabara, ambapo fedha hizo ni sehemu ya bajeti ya shilingi bilioni 18.6 zilizotengwa kwa ajili ya kazi za matengenezo ya barabara kwa mwaka wa fedha 2025/26.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa TANROADS mkoa wa Dodoma, Mhandisi Colman Ramadhani, wakati wa ukaguzi wa barabara ya Dodoma–Mtera yenye urefu wa km 140.6 uliofanywa na Wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, ikiwa ni sehemu ya ufuatiliaji wa kawaida wa utekelezaji wa kazi za matengenezo ya miundombinu ya barabara na tathmini ya maendeleo ya miradi ya matengenezo ya barabara inayoendelea.
Akizungumza katika ukaguzi huo, Mhandisi Ramadhani alisema fedha zilizopokelewa zimewezesha kuendelea na utekelezaji wa kazi za matengenezo katika mtandao wa barabara unaohudumiwa na wakala huo mkoani hapa. Aidha ameeleza kuwa upokeaji wa fedha hizo umeimarisha kasi ya utekelezaji wa miradi iliyoidhinishwa chini ya bajeti ya mwaka huu wa fedha.
“Kazi za matengenezo zinaendelea katika barabara zenye jumla ya kilomita 1,707.2 pamoja na madaraja 320, ambapo mikataba 42 imesainiwa kwa ajili ya utekelezaji wa kazi mbalimbali za matengenezo” amesema Mhandisi Ramadhani.
Ameongeza kuwa barabara ya Mtera–Dodoma inakabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo ongezeko la magari ya mizigo, hususan yale ya mazao na madini, ambapo huchangia kuharakisha uchakavu wa tabaka la juu la barabara na kuongeza gharama za matengenezo.Ametaja changamoto nyingine kuwa ni athari za mvua kubwa na mafuriko, hasa katika eneo la Manzase, ambapo maji huvuka juu ya tuta la barabara na kupelekea usitishwaji kwa huduma za usafiri kwa masaa matatu hadi sita kwa sababu za kiusalama.
Akihitimisha wasilisho lake Mhandisi Ramadhani amesisitiza kuwa TANROADS mkoa wa Dodoma itahakikisha kuwa fedha zinazotolewa na Mfuko wa Barabara kwa ajili ya kazi za matengenezo ya barabara zinatumika kwa ufanisi ili kuboresha hali ya mtandao wa barabara mkoani hapa na kuhakikisha kuwa usafiri wa barabara unakuwa salama na wa uhakika.
Zoezi la siku moja la ukaguzi wa hali ya barabara na kazi za matengenezo ya barabara ya Dodoma - Mtera limefanywa na wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara, wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Mussa Nattyna Kaimu Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Barabara na raisi wa Chama cha Mifuko ya Matengenezo ya Barabara Afrika (ARMFA), Mhandisi Rashid Kalimbaga.