Habari

Imewekwa: Sep, 20 2025

​Zingatieni Ubora Kwenye Matengenezo ya Barabara

News Images


Kaimu Mtendaji Mkuu, Mfuko wa Barabara Mhandisi Rashid Kalimbaga ametoa rai kwa wasimamizi wa TANROADS mkoa kuzingatia ubora kwenye Miradi ya Dharura ya mategenezo ya barabara (CERC PROJECT) inayoendelea katika mikoa yao ili kuhakikisha viwango vya ubora kwenye matengenezo hayo vinafikiwa kama ilivyopangwa.

Mhandisi Kalimbaga ametoa wito huo, Septemba 19,2025 wakati wa ziara ya kikazi ya siku moja ya wajumbe wa Bodi ya Mfuko wa Barabara ya kukagua miradi ya dharura ya matengenezo ya barabara inayofanyika jijini Arusha ambapo amesema Miradi yote inafanywa na wakandarasi wazawa hivyo anatoa wito kwa wasimamizi wa TANROADS Mkoa kuhakikisha wakandarasi wanafanya kazi kwa weledi na umahiri.

"Sera ya Mfuko wa barabara ni kuhakikisha Miradi yote ya Mfuko inafanywa na wakandarasi wazawa, hivyo natoa wito kwa wasimamizi wa TANROADS Mkoa kuwasimamia kwa karibu wakandarasi hao ili kuhakikisha matengenezo ya barabara yanafanyika katika ubora uliopangwa" amesema Mhandisi Kalimbaga

Kwa upande wake Mhandisi Regnald Massawe, Meneja wa TANROADS Mkoa wa Arusha amesema kama mkoa wanatekeleza miradi mitatu ya matengenezo ya barabara na miradi yote ipo kwenye hatua nzuri za utekelezaji.

"Mkoa wa Arusha tumepata Billion 11, kwaajili ya kutekeleza miradi mitatu. Hapa tupo kwenye mradi wa barabara ya Arusha - Moshi ambao umeshatekelezwa kwa asilimia 90 na kama unavyoona mkandarasi yupo site kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati na kwa ubora ubora" amesema Mhandisi Massawe

Naye Mhandisi Martin Buchardi, Mkandarasi mzawa kutoka Abemulo Contractors LTD anaefanya mradi wa maboresho ya barabara kuu ya Arusha - Moshi amesema mradi upo kwenye hatua za mwishoni na wanatarajia kuukamilisha mwezi Octoba mwaka huu kama ilivyopangwa.

Barabara kuu ya Arusha - Namanga na Barabara kuu ya Arusha - Minjingu ni Miradi mingine ya Dharura ya matengenezo ya barabara inayotekelezwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ufadhili wa Benki ya Dunia, hapa Mkoani Arusha.